Bunge la Libya limeshindwa kuidhinisha tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi wa rais ulioahirishwa wiki iliyopita, hatua inayoacha maswali kuhusu hatma ya uchaguzi huo uliotazamiwa kufanyika Desemba 24, mwaka huu, na hivyo kuwa njia ya kuelekea upatikanaji amani nchini humo.
Hapo jana kamati ya bunge iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi huo, iliwasilisha ripoti ikisema itakuwa hatari kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi na badala yake ikapendekeza kufanyiwa kazi changamoto zilizopelekea kuahirishwa uchaguzi wa Desemba 24.
Uamuzi huo ni kinyume na pendekezo la Tume ya Uchaguzi nchini Libya iliyotaka uchaguzi mwingine uandaliwe Januari 24 mwaka ujao.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na ripoti ya kamati ya bunge ni kuundwa Tume ya kubadili Katiba na kubadilishwa kwa serikali ya mpito ya waziri mkuu, Abdulhamid Dbeibah, iliyopaswa kumaliza muhula wake baada ya uchaguzi uliofutwa.
