
Maombolezo ya kifo cha mwanaharakati wa muda mrefu dhidi ya ubaguzi wa rangi, Askofu Desmond Tutu, yanaendelea nchini Afrika Kusini.
Askofu Tutu aliyefariki dunia Jumapili akiwa na umri wa miaka 90, katika siku ya kwanza ya maombolezo ya kitaifa jana Jumatatu, kengele za kanisa kuu mjini Cape Town la mtakatifu George, ziligongwa kwa dakika 10 kama heshima kwake huku raia wakijitokeza kwa wingi kuweka mashada ya maua na salamu za rambirambi nje ya kanisa hilo.
Mjane wa kiongozi wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela, Bibi Graca Machel ametoa salamu zake za rambi rambi akimwelezea askofu Tutu kama moja ya viongozi wa kizazi cha Waafrika waliojitolea kupigania maslahi ya wengi na kuwa tunu kwa bara hilo na ulimwengu kwa jumla. Hapo kesho mjini Pretoria kutakuwa na ibada ya taifa ya kumuaga kiongozi huyo wa kiroho ambaye atazikwa Januari Mosi katika viunga vya kanisa la mtakatifu George, mjini Cape Town.
