
Rais wa Marekani, Joe Biden, ameahidi kukabiliana na uhaba wa vipimo vya Covid-19 wakati kirusi kipya cha Omicron kinatishia kuzielemea hospitali na kuvuruga mipango ya safari ya maelfu ya watu nchini humo.
Akizungumza katika kikao na kamati ya taifa ya kupambana na janga la virusi vya corona pamoja na magavana wa majimbo ya Marekani, Biden amesema ni wazi idadi ya vipimo haitoshi na ni lazima serikali ifanye kazi ya ziada kumaliza upungufu uliopo.
Biden amesema miongoni mwa hatua anazochukua ni pamoja na kutumia sheria ya uzalishaji kwa ajili ya ulinzi inayoyataka makampuni ya Marekani kuitikia mwito wa serikali wa kuzalisha kwa wingi bidhaa zinazohitajika katika nyakati za dharura.
Marekani inapambana kudhibiti kishindo cha kuongezeka kwa visa vya Covid-19 ambavyo vimepanda baada ya Christmasi huku idadi ya watu wanaolazwa hospitali pia ikiongezeka.
