
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetangaza awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2022/2023 utakaokuwa kwa siku sita kuanzia leo Agosti 24 hadi Septemba 6, mwaka huu.
Hivyo, imewasisitiza waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili ama kudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali kutumia fursa hiyo kutuma maombi ya udahili kwa vyuo wanavyovipenda.
Katibu Mtendaji wa TCU, Prof.Charles Kihampa amesema hayo leo Agosti 24,2022, alipokuwa akitangaza kukamilika kwa udahili wa awamu ya kwanza na kufunguliwa kwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza 2022/2023
Kutokana na kufunguliwa awamu ya pili, tume pia imezielekeza taasisi za Elimu ya juu kutangaza programu ambazo bado zina nafasi huku waombaji wa vyuo pia wakihimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili.
“Waombaji na vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyotolewa na TCU kama inavyooneshwa kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz)”. Amesema Prof. Kihampa.
Aidha amesema katika awamu ya kwanza ya udahili, waombaji 106,295 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 76 vilivyoidhinishwa kudahili huku programu 757 zikiwa zimeruhusiwa kudahili ukilinganisha na programu 724 mwaka 2021/2022.
Amesema mwaka huu kuna nafasi 172,168 ikilinganishwa na nafasi 164,901 kwa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la nafasi 7,267 za shahada ya kwanza ambazo ni sawa na asilimia 4.4
Amesema katika awamu hii ya kwanza ya udahili waombaji 75,163 sawa na asilimia 70.71 wamepata udahili vyuoni, mwenendo huo wa udahili wa awamu ya kwanza kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019 hadi 2022/2023) unaoonesha ongezeko kubwa la waombaji na ni kiashiria cha ongezeko la wahitimu wa kidato cha sita na wale wa stashahada,
Aidha, Tume imewataka waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kuthibitisha udahili wao kwa kuchagua chuo kimojawapo kuanzia leo Agosti 24, 2022 hadi Septemba 6 2022 kwa kutumia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.
Pia TCU imewaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
