Kampuni ya Amazon ya nchini Marekani imesema itawalipia usafiri wafanyakazi wake nchini humo ambao husafiri kwa matibabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji mimba wa hiari.
Ujumbe kwa wafanyikazi wa Amazon ulisema kwamba kampuni hiyo italipa hadi dola za Marekani 4,000 au 3,201 kwa gharama za usafiri kila mwaka kwa matibabu ambayo hayapatikani karibu.
Hii inakuja wakati ambao kuna ongezeko la vikwazo vya utoaji mimba nchini Marekani. Mpango huo mpya wa Amazon utaanza kutumika kuanzia Januari Mosi, mwaka ujao.
Kulingana na tangazo hilo, lililoripotiwa kwa mara ya kwanza na Reuters, manufaa mapya yatatumika kwa matibabu ambayo hayapatikani ndani ya eneo la maili 100 kutoka katika nyumba ya mfanyakazi na ambayo huduma za mtandaoni hazipatikani.
Msemaji wa Amazon alithibitisha mpango huo kwa BBC na kusema pia unajumuisha huduma za afya ya watoto, saratani, matatizo ya kuzaliwa ndani ya miezi 24 baada ya kuzaliwa, matibabu ya afya ya akili na huduma za matatizo ya madawa ya kulevya Amazon ni moja ya waajiri wakubwa wa sekta ya kibinafsi nchini Marekani, ikiwa na wafanyakazi milioni 1.1 wa kudumu na wa muda nchini humo.
Manufaa hayo yatapatikana kwa wafanyakazi wote waliojiandikisha katika mipango miwili tofauti ya afya inayotolewa na kampuni, ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi ofisini au katika maghala. Kampuni hiyo pia inatoa hadi dola 10,000 kwa masuala ya dharura na yanayotishia maisha.
Lakini Kampuni hiyo inasema manufaa hayo hayalengi kuruhusu utoaji mimba, bali yamekuja wakati serikali za majimbo kadhaa ya Republican kupitisha sheria zinazozuia utoaji mimba katika mamlaka zao.
