
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amerejea mwito wake wa kumtaka rais Vladimir Putin wa Urusi kuacha kuishambulia Ukraine huku akiapa kwamba iwapo hilo halitakomeshwa Moscow haipaswi kushinda vita hiyo.
Akizungumza na shirika la utangazaji la ZDF Scholz amemsihi rais Putin kuondoa vikosi vyake nchini Ukraine ili kumaliza vita ambavyo tayari vimegharimu maisha ya maelfu ya watu na kuzusha mzozo mkubwa wa wakimbizi barani Ulaya.
Kansela Scholz pia ametumia nafasi hiyo kutetea sera za serikali mjini Berlin kuhusiana na vita inayoendelea akipuuza ukosoaji kuwa Ujerumani inajivutavuta kuisadia kikamilifu Ukraine kujihami dhidi ya hujuma za Urusi.
Scholz amesema msaada wa kifedha na kijeshi ambao Ujerumani na mataifa washirika yamekuwa yakiutoa kwa Ukraine ndiyo umesaidia kwa sehemu kuviwezesha vikosi vya nchi hiyo kuendelea kuwa imara mbele ya jeshi la Urusi.
