Benki ya CRDB imesema malipo yote yahusuyo msimu kwenye kombe la shirikisho iliyakabidhi kwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kama makubaliano ya kimkataba baina yao yanavyotaka.
Kupitia taarifa iliyotolewa na benki hiyo leo Juni 10 imesema “Tungependa kuufahamisha umma na wadau wote wa soka kuwa Benki ya CRDB ni taasisi yenye kuzingatia weledi, kanuni na taratibu na kwa msingi huo tayari Benki ilikwisha tekeleza kikamilifu wajibu wake wa kifedha kwa TFF kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano haya. Malipo yote ya msimu uliopita yalifanyika kwa TFF kwa mujibu wa mkataba baina ya Benki ya CRDB na TFF.”
Benki hiyo imelazimika kutoa ufafanuzi baada ya Msemaji wa Klabu ya Yanga Ali Kamwe kutangaza kuwa klabu hiyo haitoshiriki mchezo wa fainali baina yake na Singida Black Stars uliopangwa kuchezwa Zanzibar mpaka pale CRDB na TFF watakapowalipa fedha zao za ubingwa wa msimu uliopota.
