
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amezindua kampeni ya ugawaji madawati 1,000 yaliyofadhiliwa na Benki ya Exim Tanzania kwa ajili ya shule za msingi katika mikoa mbalimbali ikiwamo Dodoma, Mtwara, Lindi, Mbeya, Mwanza na Tanga.
Hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kukabiliana na uhaba wa madawati katika baadhi ya shule hapa nchini sanjari na kuboresha sekta ya elimu.
Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika mkoani Lindi jana na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwamo viongozi waandamizi wa serikali, baadhi ya wabunge wa mkoa huo, wananchi, wanafunzi pamoja na viongozi wa benki hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema hatua hiyo itasaidia sana kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoketi sakafuni huku akibainisha kuwa serikali inaendeleza jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wadau kumaliza changamoto hiyo.
Wakati wa hafla hiyo Waziri Mkuu Majaliwa alimkabidhi mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainab Telack, madawati 200 kwa ajili ya mkoa wa huo ikiwa ni sehemu ya mpango huo huku akiwaomba wadau mbalimbali kuiga mfano wa benki ya Exim kwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono jitihada hizo.
Awali akizungumza kuhusu kampeni hiyo, ofisa mtendaji mkuu wa Benki hiyo, Jaffari Matundu, alisema ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika kusaidia jamii unaofahamika kama Exim Cares na ni dhamira ya benki hiyo katika kuisaidia serikali kukabiliana na upungufu wa madawati katika baadhi ya shule hapa nchini.
