
Jamii imeshauriwa kula uyoga kwa wingi ili kunufaika na protini zilizosheni ndani yake ambazo zinasaidia kuongeza kinga za mwili, kuondoa magonjwa ya ngozi na mapunye.
Mtaalam wa Virutubisho Tiba, Abdallah Mandai, ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 28, 2021, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia makundi mbalimbali ya vyakula na umuhimu wake kwa mwili wa binadamu.
“Ubora wa uyoga upo katika ule mbichi. Ili kupata protini kutokana na uyoga, tengeneza juisi ya uyoga mbichi, kunywa inasaidia kuondoa tatizo la koo, maradhi ya tumbo, ukungu katika mapafu, ni tiba ya kidonda kibichi na tatizo la pumu.
“Chakula hiki pia ni lishe nzuri kwa wagonjwa wanaougua magonjwa ya muda mrefu hususan wale walio kitandani, juisi ya uyoga itampa uwezo na nguvu ya kutembea kwa haraka zaidi.
“Uyoga unapokula kama mboga una faidika na viini lishe vingi muhimu kwa afya ya binadamu, licha ya wingi wa protini, una vitamini A, B, C na K. Pia una madini yanayohitajika katika mwili wa binadamu.
“Ni vema tujenge utaratibu katika familia wa kula uyoga mara kwa mara ili kunufaika nao. Zao la uyoga pia lina faida kwa kuwa linaongeza pato la familia,” amesema Mtaalam Mandai.

Ametanabahisha kuwa uyoga ule wenye rangi ya udongo na nyekundu kidogo ni mzuri zaidi kwamba Tanzania ina utajiri wa uyoga asili unaoota kwa wingi kipindi cha mvua za masika.
