JUMLA ya watahiniwa 557,731 leo Jumatatu Novemba 11 wameanza kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne ambapo kati yao 529,321 ni wa shule na watahiniwa wa kujitegemea ni 28,410
Mtihani huo utafanyika katika shule za sekondari 5585 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 961 .
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt. Said Mohamed amesema hayo Novemba 10, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo.
Dkt Mohamed amesema katika watahaniwa wa shule 557,731 waliosajiliwa kufanya mtihani huo wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66.
“Aidha watainiwa wa shule wenye mahitaji maalum 1,088 waliosajiliwa kati yao 601 ni wenye uoni hafifu, 56 ni wasioona, 209 wenye ulemavu wa kusikia, 39 ni wenye ulemavu wa akili na 183 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,”amesema Mohamed
Amesema, Watahiniwa wa kujitegemea 28,410 wamesajiliwa ambapo kati yao wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana 17,243 sawa na asilimia 60.69 huku kwa wenye mahitaji maalum wakiwa 18 kati yao mwenye uoni hafifu ni mmoja, wasioona 16 na mwenye ulemavu wa viungo mmoja.
