
Msimamizi wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU)
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prisca Kiyuka akielezea huduma
zinazotolewa kwa wagonjwa waliotoka kufanyiwa upasuaji wa moyo na
kufikishwa katika chumba hicho kwa wageni kutoka Taasisi ya Moyo ya Uganda
walipotembelea JKCI kwa ajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo
pamoja na kujifunza namna ambavyo Taasisi hiyo inaendesha shughuli zake (PICHA YA JKCI).
Wataalam wa afya 20 kutoka Taasisi ya Moyo Uganda wametembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ya jijini Dar es Salaam.
Leo la ziara hiyo ni kujifunza huduma za matibabu ya moyo zinavyotolewa pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo inavyoendesha shughuli zake.
Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Juni 28, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi amesema baada ya kusikia mafanikio yaliyopatikana katika Taasisi hiyo wataalamu hao kutoka nchini Uganda wameona ni vema waje nchini kujifunza mafanikio hayo pamoja na changamoto zake ili nao wafikie hatua kama ya JKCI.
Prof. Janabi amesema tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 2016 imekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji huduma za matibabu ya moyo kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 8663 na kuona wagonjwa zaidi ya laki sita na hivyo kuwa hospitali bora ya Serikali inayotoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
“Mwaka 2017 baadhi ya wabunge kutoka nchini Uganda walitembelea Taasisi yetu kwa ajili ya kujifunza na leo hii tumepokea wataalamu 20 kutoka nchini humo ambao nao wamekuja kujifunza jinsi tulivyofanikiwa katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo. Sisi tumefanikiwa kwa kuwa Serikali inatuunga mkono kwa zaidi ya asilimia 120 na hata upasuaji tunaoufanya ni salama.
“Taasisi yetu inapokea wagonjwa kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na Kati ikiwamo Uganda ambapo kwa mwaka huu tumeshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto sita ambao walikuwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo. Watoto hawa wanaendelea vizuri na walisharudi nchini mwao,” amesema Prof. Janabi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI Prof. William Mahalu amesema amefurahi kuona wenzao kutoka Uganda wamekuja kuwatembelea kwa ajili ya kujifunza wanachokifanya na kuwaeleza walipofikia ili wawasaidie kutokana na mapungufu waliyokuwa nayo.
“Ukiangalia historia ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete haitofautiani na ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo Uganda kwani zote zimetokea katika Hospitali za Taifa, jambo muhimu ni kuwatia moyo ili wasikate tamaa na kuweza kufika hapa tulipofika sisi kwani wao wako hatua tatu nyuma yetu.
Dk. James Magara ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Moyo Uganda amesema wamekuja nchini kujifunza katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ili wasifanye makosa kiutendaji kwani wao wako katika hatua za mwanzo tangu taasisi hiyo ianzishwe na kama wataanza vizuri wataweza kufanya vizuri zaidi.
“Tanzania na Uganda tumekuwa na uhusiano mzuri tangu miaka ya nyuma, tumefaidika na Tanzania kwani wakati wa vita vya Idd Amin Tanzania ilikuja kutusaidia. Na sisi leo tumekuja kujifunza kwa wataalamu wenzetu kuona ni vitu gani wamevifanya na kuweza kufikia hatua hii kwani kuwa na Taasisi kama JKCI siyo kitu cha muda mfupi,” amesema Dk. Magara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Uganda, Dk. John Omagino amesema Serikali ya nchi hiyo imeamua kujenga kituo cha matibabu ya moyo ili kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Pia kituo hicho kiwe na ubora sawa na vituo vingine vya Afrika Mashariki ili wagonjwa wa moyo watibiwe ndani ya nchi hizo.
Amesema taasisi yao bado ni ndogo na wanatakiwa kusonga mbele zaidi, Serikali yao imewapa ardhi na wamepata fedha ambazo zitawawezesha kujenga jengo kubwa la Taasisi hiyo hivyo basi ili waweze kufanya kitu kizuri wameona watembelee vituo vingine vya moyo vilivyopo Afrika Mashariki na kujifunza vitu ambavyo vimewafanya wamefanikiwa hii ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu wa afya.
Wataalamu hao ambao ni wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Uganda wameambatana na watunga sheria na sera watakuwa katika Taasisi hiyo kwa muda wa siku mbili na watatembelea maeneo mbalimbali ya JKCI pamoja na kuzungumza za wakuu wa idara ili waweze kubadilishana ujuzi wa kazi.
