Idara ya polisi nchini Mali imesema askari Polisi watano wa nchi hiyo, wameuawa na washambuliaji wasiojulikana Kusini mwa nchi hiyo.
Wakati hilo likiripotiwa Jeshi la Mali linadai kudhibiti shambulio tofauti la wanamgambo wa Kiislamu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kikosi kwenye kituo cha polisi cha Sona kilikanyaga kilipuzi na kulifuatia ufyatuaji mkali wa risasi uliofanywa na washambuliaji ambao hawajajulikana”, idara ya polisi imesema katika taarifa yake.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa maofisa watano wa polisi waliuawa, mmoja akajeruhiwa na wengine watatu hawajulikani aliko.
Shambulio hilo lilifanyika katika mji wa Sona, eneo la Koutiala, karibu na mpaka kati ya Mali na Burkina Faso.
Ofisa wa eneo hilo aliyechaguliwa na ofisa mmoja wa polisi ya taifa, wote wakizungumza na AFP kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wamewaelezea washambuliaji kuwa ni magaidi.
Mali inakabiliwa na uasi wa muda mrefu wa wanamgambo wa kiislamu ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kulazimisha maelfu ya wengine kuhama makazi yao.
