Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema nchi yake haitaagiza mafuta kutoka Urusi kama alivyoomba waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Uganda.
Katika hotuba yake kwa taifa, Museveni amesema licha ya Urusi kutaka kuiuzia Uganda mafuta kwa bei rahisi, na licha ya kwamba bei ya mafuta imeongezeka sana nchini Uganda, hataki “kujiingiza katika mgogoro kati ya Marekani na Urusi.
Amesema serikali itatafuta mbinu mbadala za kuhakikisha kuna mafuta ya kutosha nchini Uganda, wakati inajitayarisha kutekeleza mikakati ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuwa na nishati safi, magari na pikipiki zinazotumia nguvu za umeme.
“Endapo tutanunua mafuta kwa bei rahisi kutoka Urusi ina maana kwamba tunakiuka vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Urusi,” amesema Museveni, akiongezea kwamba “tangu tatizo lilipoanza, amekuwa akiwasiliana na viongozi wa Urusi na Marekani. Sasa mnaweza kuona mazungumzo yetu yameanza kuruhusu nafaka na ngano kusafirishwa kutoka Ukraine.”
Museveni amesisitiza kwamba njia ya kusuluhsisha uhaba wa bidhaa muhimu unaoshuhudiwa duniani kwa sasa ni kutumia diplomasia.
“Kama nataka kununua mafuta, ningeiambia Urusi kusafirisha mafuta hayo hadi hapa na wangefanya hivyo. Lakini hatua hiyo inatuweka katika matatizo na Marekani ambayo sio jambo zuri. Kwa sasa, tutumie vizuri mafuta tuliyo nayo huku tukitafuta mbinu mbadala.”
Hotuba ya Museveni kwa taifa imejiri siku chache baada ya kukutana na mabalozi wa ngazi ya juu wa Urusi na Marekani.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov alikuwa Uganda Julai 26. Alisema nchi yake ilikuwa tayari kufanya mazungumzo na Uganda, kuhakikisha inapata mafuta ya bei rahisi au nafuu ili kukabiliana na uhaba wa bidhaa hiyo nchini humo.
