
Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kiislamu wamewaua watu zaidi 130 katika miji jirani katikati mwa Mali.
Mauaji hayo yamefanyika mwishoni mwa juma ikiwa ni ya hivi karibuni katika eneo hilo la Sahel lenye mzozo.
Maofisa wa eneo hilo wameripoti matukio ya mauaji ya kiholela yaliyofanywa na watu wenye silaha huko Diallassagou na miji miwili jirani eneo la Bankass, huko Sahel ambalo limekuwa lenye machafuko kwa muda mrefu.
“Walichoma pia vibanda, nyumba na kuiba ng’ombe,” amesema ofisa wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama.
Yeye na ofisa mwingine ambao wote wawili walikimbia kijiji chao, wamesema hesabu ya watu waliouawa ilikuwa ikiendelea jana Jumatatu.
Nouhoum Togo, ofisa wa mji wa Bankass ambao ni mkubwa katika eneo hilo, amesema idadi ya waliouawa ni kubwa kuliko ile ya watu 132 iliyotangazwa na serikali, ambayo iliwashtumu wanamgambo wa kiislamu washirika wa Al-Qaeda kwa mauaji hayo.
