
Mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali za Jumuia ya Madola unafanyika jijini Kigali, nchini Rwanda.
Mkutano huo wa siku tano ulianza jana Juni 20, 2022, na unatarajiwa kufikia tamati Juni 25, 2022.
Makundi mbalimbali ya vijana, wanawake, wafanyabiashara, mawaziri wa mambo ya nje, wakuu wa nchi pamoja na mijadala, wanashirki huku ukijikita katika maeneo matano.
Aidha, mkutano huo unafanyika sasa baada ya kuahirishwa mara mbili (2020 na 2021) kwa sababu ya ugonjwa wa Corona.
Mkutano huo pia utajikita katika maeneo ya utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu; vijana, afya, teknolojia na uvumbuzi, maendeleo endelevu na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo uliobeba kauli mbiu ‘Kufikia mustakabali wa pamoja, kuunganisha, kufanya uvumbuzi na mabadiliko” umejikita katika kujadili na kutafutia ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili nchi wanachama wa Jumuia hiyo ili kufikia maendeleo ya kweli katika nyanja zote.
Tanzania inashiriki mkutano huo na kimsingi masuala yanayojadiliwa yanakwenda sanjari na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
