
Vikosi vya serikali ya Somalia vimemaliza uvamizi wa zaidi ya saa tano wa jengo lenye ofisi ya Meya wa Mogadishu na vituo vingine vya serikali ya wilaya.
Wizara ya habari, utamaduni na utalii imesema maofisa usalama waliwaua wapiganaji sita wa Al-Shabab waliohusika katika shambulio hilo la jana Jumapili.
Raia watano waliuawa pia na wengine wanne kujeruhiwa, taarifa ya wizara hiyo imeongeza.
Serikali ya Somalia imesema washambuliaji wa al-Shabab walifika kwenye jengo hilo kwa mguu, wakijifanya askari wa serikali.
Shambulio hilo lilianza na mlipuko uliofuatwa na uvamizi wa jengo hilo uliofanywa na watu wenye silaha.
“Majira ya saa sita mchana, walishambulia kwa bomu lango la nyuma lililo mbele ya wilaya ya Hamarweyne,” Naibu Meya Isse Gure amesema.
Gure ameiambia VOA kwamba maofisa wa serikali ya wilaya isipokuwa Meya Yusuf Hussein Jimale walikuwa kwenye jengo hilo wakati shambulio lilipotokea. Jimale yuko nje ya nchi.
