
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amerudia tena msimamo wake kwa Finland na Sweden kujiunga na Nato na ametoa saa kadhaa tu baada ya nchi hizo kusema kuwa zitaomba uanachama.
Amesema nchi hizo mbili za Kiscandinavia hazihitaji kutuma wajumbe kuishawishi Uturuki, mjumbe muhimu wa Nato, kuhusu azma yao.
Anakasirishwa na kile anachokiona kama utashi wa nchi hizo wa kuwapokea wanamgambo wa Kikurdi.
Awali Sweden ilisema Ulaya inaishi katika hatari mpya halisi ikimaanisha uvamizi wa Urusi katika Ukraine.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema hatua ya Finland na Sweden ya kujiunga na muungano wa kijeshi wenye wanachama 30 haiitishi Moscow moja kwa moja- lakini akasisitiza kuwa kupanuka kokote kwa miundo mbinu ya kijeshi kunaweza kuibua jibu kutoka kwa Urusi.
Katika mkutano wa waandishi wa habari Jumatatu, Erdogan alisema Uturuki inapinga azma za Finland na Sweden za kujiunga na Nato, akiielezea Sweden kama kitovu cha mashirika ya ugaidi.
“Hakuna nchi moja kati ya hizi ambayo ina mtizamo wa wazi, kuhusu mashirika ya ugaidi. Tunawezaje kuwaamini ?,” Rais wa Uturuki amesema.
