
Ikiwa leo ni siku ya maziko ya mtoto Erickson Kimaro (8), anayedaiwa kunyongwa na mfanyakazi wa kazi za ndani jijini Dar es Salaam, Digna Nasisiriwa mama mzazi wa marehemu huyo amesema alipomchunguza mwanawe kwa mara ya kwanza alibaini michubuko shingoni na usoni karibu na jicho.
Akihojiwa na televisheni moja jana jijini Dar es Salaam, Digna aliyeonekana amezama katika lindi la huzuni kubwa amesema alipigiwa simu na dada huyo wa kazi kuwa Erickson haamki kila anapomwamsha tangu alipolala baada ya kutoka shule.
Amesema akapiga simu shuleni ikiwa walimwona mgonjwa akajibiwa kuwa alikuwa mzima na hata alipompigia dereva wa gari la shule naye akamwambia hadi anamshusha hakuwa na dalili ya homa.
Amesema baada ya majibu hayo alimwambia tena dada amwamshe kwa kumtikisa mwili wake huku akimwita jina kwa sauti lakini akamjibu kuwa bado tu haamki.
“Nikamwambia amshike kifuani kubaini kama mapigo ya moyo yanafanya kazi na amzibe pua kubaini iwapo anapumua lakini akaniambia kuwa moyo haudundi na wala hapumui,” amesema.
Ndipo alipofika nyumbani katika kumchunguza akabaini michubuko shingoni na usoni karibu na jicho huku eneo la shingo pekee likiwa na joto ndipo akaona amkimbize hospitali ya Mloganzila.
Baba mzazi wa marehemu Dakta Erick Kimaro amesema mwanawe alipofikishwa hospitali ya Mloganzila alikuwa tayari ameshafariki dunia na kwamba walilazimika kwenda kutoa ripoti kituo cha polisi baada ya kubaini michubuko katika mwili wa marehemu.
Aidha, amemzungumzia mwanawe kuwa alikuwa ni mtoto mdadisi na mwenye akili.
“Mtoto wangu siku moja kabla ya mauti alikuwa mwenye furaha na mchangamfu kama ilivyo kawaida yake.
Erickson amefariki kifo chenye utata Jumatatu Mei 30, 2022, majira ya saa jioni baada ya kufikishwa nyumbani na gari la shule akiwa mzima wa afya na baada ya kwenda kulala kama ilivyo kawaida yake hakuamka tena.
Baba mzazi amesema camera za CCTV hazikuwashwa siku ya tukio hivyo hajui chanzo halisi cha kifo cha mwanawe huyo aliyekuwa anasoma darasa la tatu.
Erickson anatarajiwa kuzikwa leo alasiri katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, baada ya buriani itakayotanguliwa na Ibada itakayofanyika kulingana na tamaduni za Kanisa la KKKT alikokuwa akiabudu pamoja na wazazi wake wakati wa uhai wake.
