
Wizara ya Ulinzi ya Tunisia, imesema meli zake zimeokoa wahamiaji 178 waliokua wanajaribu kuvuka bahari ya Mediterranean wakitokea Libya kuelekea Ulaya.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi, imesema miili miwili ilipatikana na wahamiaji 178 waliokolewa wakati wa oparesheni tatu kwenye Pwani ya Kusini mwa Tunisia.
Wizara hiyo imesema wahamiaji hao ambao ni kutoka Misri, Tunisia, Syria, Ivory Coast, Bangladesh, Nigeria, Mali na Ethiopia, walikuwa wameondoka kutoka bandari ya Libya ya Zuwara Ijumaa usiku.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM, lilisema Alhamisi, viongozi wa Tunisia walikamata wahamiaji 267 ambao walikua wameanza kuvuka bahari kutoka Libya, wengi wao wakiwa raia wa Bangladesh.
Kwa mujibu wa na takwimu za IOM, zaidi ya wahamiaji 1,000 waliotarajia kufika Ulaya walikuwa wameondoka Libya na kuishia Tunisia tangu mwezi Januari, huku idadi ya wanaoondoka inazidi kuongezeka.
