Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema imejipanga kikamilifu kuanza uchunguzi wa kina kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ambazo zilisababisha vifo vya raia pamoja na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Novemba 5, 2025 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amesema lengo la kufanya uchunguzi huo ni kuishauri serikali ili kuweza kudhibiti matukio kama hayo katika chaguzi zijazo akisisitiza kuwa matukio ya aina hiyo hayawezi kuvumiliwa katika jamii inayothamini amani na utawala wa sheria.
“Kwa namna yoyote ile, matukio ya aina hii yaliyotokea hayapaswi kuungwa mkono, kwa sababu yanavunja amani ya nchi na kuhatarisha usalama wa wananchi. Sisi kama Tume, kutokana na matukio hayo, tumeamua kufanya uchunguzi wa kina na tayari tumejipanga vizuri kuhakikisha jambo hili linashughulikiwa ipasavyo”, amesema Jaji Mwaimu.
