
Mkazi wa mtaa wa Idofi, halmashauri ya mji wa Makambako, mkoani Njombe, Elina Nzilano (87), ameuawa na mwanawe Elisha Mwena (42), kwa kumtuhumu mchoyo.
Mwena ambaye mlemavu wa kutokuona, anadaiwa kumshambulia mama yake huyo mzazi kwa fimbo hadi kumjeruhi vibaya baada ya kile kinachodaiwa kumnyima chakula mtoto wake (mjukuu wa marehemu).
Taarifa za awali za Jeshi la Polisi mkoani Njombe zinasema mlemavu huyo alimshambulia kikongwe huyo baada ya kukasirishwa na hatua yake ya kutompa chakula mjukuu wake (mtoto wa mshukiwa).
Kamanda wa polisi Mkoa huo, Hamis Issah amesema “Sababu ya bibi kumnyima chakula mjukuu ni baada ya kumwibia kuku ambaye alimchinja na kumla peke yake kitendo kilichomkasirisha bibi huyo hadi kumnyima chakula.
Idaiwa kuwa wakati marehemu anakula chakula bila kumpa mjukuu wake mshukiwa alikuwa amekaa pembeni akisikia majibizano baina yao ambapo marehemu aliweka wazi kuwa hatampa chakula kamwe ndipo mshukiwa Elisha alichukuwa fimbo yake na kumshambulia mama yake huyo ambaye hakuwezi kujitetea kutokana na umri wake na kumjeruhi vibaya ambapo alifariki hospitali wakati akipatiwa matibabu.
Kamanda Issah amesema Jeshi lake linamshikilia mlemavu huyo kwa uchunguzi kisha sheria itachukue mkondo wake.
