
Katibu mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi amesisitiza kuwa hadi sasa nchi ipo salama hakuna kisa cha ebola kilichoripotiwa hapa nchini hivyo amewataka wataalam wa afya mipakani kuongeza kasi ya uchunguzi wa ugonjwa huo.
Prof. Makubi ametoa kauli hiyo jana Alhamis Septemba 29, 2022, akiwa wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya Bukoba.
Alifanya mazungumzo nao mara baada ya kufanya ziara maeneo ya Mtukula kukagua hatua mbalimbali za serikali ambazo zimeshaanza kuchukuliwa katika kukabiliana na Ebola ili isienee nchini baada ya kuripotiwa visa vya ugonjwa huo katika nchi jirani ya Uganda hivi karibuni.
Amesisitiza kuwa hadi sasa nchi ipo salama hakuna kisa vya ebola kilichoripotiwa hapa nchini.
“Serikali imejipanga kuhakikisha ugonjwa wa Ebola hauenei nchini na niwahakikishie Watanzania hakuna Ebola Tanzania, hatua ambazo zimeshaanza kuchukuliwa ni pamoja na kusambaza vifaa vya kupimia Ebola na magari ya kubebea wagonjwa.
“Kwa sababu kuna njia nyingi za kupita wananchi katika mipaka, nitoe maelekezo kuhakikisha kuongeza kasi ya uchunguzi katika mipaka tunaona kuna mipaka mingi wananchi wanapita,” amesema.
Kuhusu uelimishaji pamoja na kuweka vifaa muhimu vya kupima Ebola Prof. Makubi amesema Wizara ya Afya imejipanga ambapo jopo la wataalam kutoka wizarani kwa kushirikiana na wataalam wa afya kutoka mikoa ya mipakani wameendelelea kutoa elimu ambapo ameagiza kuongeza kasi ya uelimishaji zaidi kwa njia ya vyombo vya habari na vipeperushi.
Hivyo, ameendelea kusisitiza kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwamo kunawa mikono mara kwa mara.
Nao baadhi ya wananchi mkoani Kagera wameishukuru serikali kwa kuendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na Ebola huku wakiomba ukaguzi kuendelea kuimarishwa zaidi sehemu za mipaka.
