
Rais Samia Suluhu Hassan, amewashukuru maaskofu Katoliki kwa kuwa pamoja na serikali katika kipindi cha msiba wa Rais wa Awamu wa Tano, Hayati Dakta John Magufuli, kilichotokea Machi 17, mwaka huu.
Ametoa shukrani hizo leo katika mkutano wake na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), uliofanyika kwenye makao makuu ya Baraza hilo, Kurasini, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yake Rais Samia amesema anawashukuru pia kwa kumpa pongezi za kushika madaraka hayo ya urais ambayo ameyaelezea kuwa ni magumu mno hasa katika kipindi cha mwanzo.
Amebainisha kuwa alikubali mwaliko huo ambao awali alipopewa taarifa alisita, ili pamoja na mambo mengine kuja kutoa shukrani za serikali kutokana na kazi mbalimbali za kuliendelea Taifa zinazofanywa na kanisa hilo nchini.
Kwa upande wake Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, amemshukuru Rais Samia kwa kukubali kukutana na Baraza hilo na kuelezea kuwa kukubali kwake ni heshima kubwa sana kwa baraza hilo.
Pia amesema ni ishara ya wazi kuwa anathamini Baraza hilo, hivyo amempongeza kwa kuwa rais wa kwanza mwanamke kuongoza nchi, kuongoza kipindi cha mpito kutoka serikali ya awamu ya Tano hadi Sita kwa utulivu na amani na kuimarisha utetezi na ulinzi wa haki za binadamu kwa njia mbalimbali.
Amesema TEC inamshukuru Mungu kwa kukubali Rais Samia awe kiongozi wa Tanzania wakati huu hivyo inamwombea hekimana busara ili aendelee kulitumia taifa kwa weledi.
