
Waziri wa Fedha na Mipango, Dakta Mwigulu Nchemba, amesema ipo haja kwa watoto wadogo kuanza kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ili wanavyokua wafahamu ukwepaji kodi au upokeaji na utoaji rushwa ni kitendo cha aibu katika familia na Taifa.
Dakta Mwigulu ametoa kauli hiyo jana Juni 24, 2021, Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa Taifa linalojengwa na watu wa aina hiyo linakuwa bora na imara.
Amefafanua kuwa hali ilivyo sasa nchini, jamii nyingi hazioni kosa kujihusisha na masuala ya kutoa na kupoa rushwa pamoja na ukwepaji kodi. Aidha, amesema Wizara yake inaendelea kuzungumza na Wizara ya Elimu kuangalia namna Tanzania inavyoweza kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa na ukwepaji kodi kuanzia wakiwa na umri mdogo ili kujenga kizazi chenye maadili mema tangu utotoni.
