
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameitaka serikali kuwaelekeza madereva wa viongozi wakiwamo mawaziri kuzima magari na kushuka mara baada ya kufika maeneo husika.
Dk. Tulia ameyasema hayo leo Mei 17, 2022, Bungeni jijini Dodoma, baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Spika amesema madereva wa viongozi bado walikuwa wakiendelea kubaki kwenye magari huku yakiwa yana unguruma licha ya viongozi kuwako bungeni.
“Katika juhudi zinazofanywa na serikali za kubana matumizi, liko jambo nimekumbushwa mapema leo.
“Magari ya viongozi ikiwa ni pamoja na ya mawaziri na naibu mawaziri yanaendelea kuwaka hapo nje wakati sisi tuko humu ndani.
“Waheshimiwa wabunge mjue, lakini pia upande wa serikali tunatamani magari ya viongozi yakisha mshusha kiongozi bungeni ama nchi nzima ikishamshusha awe ni katibu mkuu awe meya au kiongozi yeyote ukiacha viongozi ambao kwa itifaki yao magari yao yanapaswa kuendelea kuwaka ni matumizi mabaya ya fedha za serikali,” amesema Spika Tulia.
