Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema bado kimeendelea kusisitiza kuhusu msimamo wake wa Jana Aprili 18, 2025 wa kulitaka Jeshi la Magereza na Vyombo vingine vya Dola kueleza kwa “haraka” alipo Mhe. Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, wakieleza kuwa mara baada ya saa 24 kupita, wataeleza umma kuhusu hatua zitakazofuata ikiwa bado haitokuwa inajulikana alipo Mhe. Tundu Lissu.
Kauli ya Chadema kupitia kwa Mkurugenzi wake wa uenezi na Mawasiliano Bi. Brenda Rupia inakuja takribani saa 18 tangu kuchapishwa kwa Taarifa yake kwa Vyombo vya habari, ambapo mpaka sasa si Jeshi la Magereza, serikali ama chombo chochote cha Dola kilichoeleza alipo Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, zaidi ya kile kilichozungumzwa mapema Jana na Msemaji wa Magereza Bi. Elizabeth Mbezi aliyekiambia chombo kimoja cha habari kuwa ingali Jeshi hilo linafuatilia kujua kilichotokea.
Lissu amekuwa akishikiliwa mahabusu katika Gereza la Keko lililopo jijini Dar Es Salaam toka alipofunguliwa mashtaka ya uhaini juma lililopita na Chadema ililitaka jeshi la Magereza, mamlaka husika na vyombo vya dola kutoa taarifa wazi na haraka kwa umma kuhusu mahali alipopelekwa Bw. Lissu.
Kando ya Jeshi la Magereza, Kulingana na BBC Swahili, Msemaji wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa alipoulizwa kuhusu madai ya viongozi wa Chadema na familia kuzuiwa kumuona Lissu na taarifa kuwa ametolewa gerezani, Msigwa naye alijibu kusema kuwa maswali hayo waulizwa Jeshi la Magereza.
