
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ametoa mwito kwa wananchi wa kitongoji cha Chihikwi, kata ya Mbarawara, jijini Dodoma, kusubiri majibu ya Serikali kuhusu mgogoro wa ardhi kati yao na Jeshi la Magereza.
Mgogoro huo wa ardhi ambao ni wa miaka minane, umemfanya Simbachawene kwenda katika kitongoji hicho kukaguzi eneo lenye mgogoro na baadaye kuzungumza na wananchi ambapo aliwapa fursa ya kutoa maoni na kero zao.
Akizungumza baada ya kuwasikiliza, Waziri Simbachawene amesema anakwenda kutafakari na kufanyia kazi malalamiko yote yaliyotolewa na atarudi kutoa majibu kwa wananchi hao na yatazingatia umuhimu wa pande zote mbili.
Amesema licha ya kuwa anatarajia kuja na majibu ya maoni hayo lakini wananchi wanapaswa kujua kuwa ardhi ni mali ya umma, kama serikali inaweza kuichukua kwa ajili ya masuala ya umma wanapaswa kupisha na pia wana haki ya kulipwa fidia kwa kile walichokiendeleza katika ardhi na siyo vinginevyo.
Akizungumzia mgogoro huo, mkazi wa kitongoji hicho, Elias Kapugi, aliiomba Serikali kuwafikiria wakati wanataka kuwaondoa katika eneo hilo kwasababu wao wanafamilia na watoto wamekuwa wakubwa, hivyo kutoa robo eka kwa kila kaya sio sahihi, hivyo wanaomba waliofikisha umri wa miaka 18 nao wapewe eneo.
Naye Diwani wa kata ya Mbarawara, Charles Ngambi, amewataka wananchi hao kutulia wakisubiri maelekezo ya Serikali yenye uamuzi utakaozingatiwa na pande zote mbili.
