
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, amelaani kitendo cha watu wasiojulikana kuwatisha wanahabari wa ITV, TBC na Mwananchi.
Akizungumza leo Juni 24, Mukajanga amesema Baraza limepokea taarifa hizo kwa mshtuko mkubwa hasa ikizingatiwa Mei 20, 2021 katika Mkutano Mkuu wa Wahariri mjini Morogoro, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Serikali haitakubali kuona waandishi wa habari wakinyanyaswa.
Katika hotuba yake hiyo, Waziri Mkuu alibainisha kuwa siyo sera ya Serikali kunyanyasa waandishi wa habari hapa nchini.
Wanahabari wa vyombo hivyo wametishiwa na watu wasiojulikana kutokana na kuandika habari zinazomhusu aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aliyefikishwa mahakamani akituhumiwa kutenda kwa makosa mbali mbali.
