
Mkuu ma mkoa wa Ruvuma, Brigedia Generali Wilbert Ibuge, amewaagiza viongozi wa wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, kutekeleza maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, kabla ya Septemba 30, mwaka huu.
Brigedia Ibuge amesema ni vema kabla ya kufikia wakat huo viongozi wawe wametekeleza maagizo ya kamati ya kudumu ya bunge pamoja na kuhakikisha hoja ambazo hazijafungwa zinafungwa.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani ambacho pamoja na mambo mengine kilijadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kuhusu hoja na mapendekezo yake.
Amesema Katibu Tawala wa mkoa huyo, Stephen Ndaki awasilishe taarifa ofisini kwake za namna alivyosimamia halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kutekeleza maagizo ya kamati ya kudumu ya bunge pamoja na kufunga hoja ambazo hazijafungwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo imepata hati yenye mashaka na msingi wake ni kutokana na sababu ya hati za madai zilizoidhinishwa kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato (LGRCIS) bila kuwa na nyaraka toshelezi ya shilingi 191,935,660.
