
Rais wa Tunisia Kais Saied amelivunja bunge la nchi hiyo na kusema kwamba wabunge watafunguliwa mashtaka.
Alilivunja jana Jumatano huku akijiongezea mamlaka zaidi kwa kipindi cha miezi 8. Hali hiyo inatajwa kuongeza zaidi mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Alitoa taarifa hiyo kwenye mkutano na baraza la usalama wa kitaifa, saa chache baada ya wabunge kufanya kikao kwa njia ya mtandao na kupitisha muswada wa sheria unaopinga hatua za dharura zilizochukuliwa na rais Saied mwaka jana.
βLeo, katika wakati huu wa kihistoria, natangaza kuvunja bunge la wawakilishi wa wananchi, ili kuilinda nchi na taasisi zake,β alisema katika taarifa yake iliyopeperushwa kwenye televisheni ya taifa hilo.
Amelaani hatua ya bunge na kuitaja kuwa jaribio la mapinduzi, na kusema kwamba wahusika walilisaliti taifa.
Amesema β Watafunguliwa mashtaka ya uhalifu.β
Muhadhiri huyo wa zamani wa masomo ya sheria, ambaye alichaguliwa mwaka wa 2019 baada ya hasira ya wananchi dhidi ya wanasiasa, Julai 25, mwaka jana, aliifuta serikali, kusimamisha bunge na kujipatia mamlaka mbali mbali.
