Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amemfuta kazi Waziri wa Fedha wa nchi hiyo zaidi ya miezi miwili tu baada ya kumteua huyo akiwa ni Waziri wa nane wa Fedha kutimuliwa.
Shirika la Utangazaji la Sudan Kusini lilitangaza kwamba Kiir amemuondoa Athian Diing Athian katika nafasi yake kama Waziri wa Fedha, na kumteua Barnaba Bak Chol badala yake.
Kiir ameongoza Serikali ya mpito tangu Uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.
Uchaguzi uliopangwa umeahirishwa mara mbili, na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, mpinzani mkuu wa Kiir wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013-2018, alishtakiwa mapema mwaka huu kwa uhaini.
Hakuna sababu iliyotolewa kwa mabadiliko ya nane ya Waziri wa Fedha tangu 2020. Barnaba Bak Chol alishikilia wadhifa huo kwa takriban nusu mwaka hadi alipofutwa kazi mnamo Machi 2024.
Kiir, siku za nyuma, aliwafuta kazi ghafla Maofisa Wakuu katika Serikali yake bila kutoa sababu.
