
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hatarajii kuona mkuu wa mkoa anakuwa mla rushwa au anageuka mungu mtu katika mkoa wake.
Hali kadhalika amewataka viongozi wa serikali kwenda kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo kwa taifa kwa kuwa ndilo kusudio la Chama Cha Mapinduzi.
Mama Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 11, 2021, katika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwemo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema.
“Uongozi ni dhamana siyo zawadi..tunategemea viongozi mtakuwa mfano, sitegemei kuona mkuu wa mkoa anaingia kwenye vitendo vya rushwa.
“Sitegemei kuona wakuu wa mikoa mnakuwa miungu watu huko mliko, mpo kule kutumikia watu, siyo watu wawatumikie ninyi. Naomba mkafanye kazi tulizowatuma.
“Ninakotoka hakuna makabila, mimi sina kabila, mwalimu Nyerere hakuwa na kabila.. kwenye utendaji wangu wa kazi ukilikoroga nakutumbua bila kuangalia kabila, anayekosea nitamuondoa, sipangi kwa kuangalia kabila, napanga kwa uwezo wake ili kwenda kusaidia wananchi kuleta maendeleo,”amesema Rais Samia.
