Maelfu ya wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bahi Mkoani Dodoma, leo Jumanne Septemba 09, 2025 wamejitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyepita wilayani humo akielekea mkoani Singida kuendelea na kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akiwa Bahi amebainisha kuwa serikali yake ya awamu ya sita imefanya vizuri kwenye utekelezaji wa huduma ya usambazaji wa maji safi na salama nchini, akisema dhamira yake ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na huduma hiyo ya uhakika ikiwa atapata ridhaa ya kuchaguliwa tena na wananchi.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 09, 2025 akiwa wilayani Bahi mkoani Dodoma kwenye muendelezo wa kampeni zake mkoani humo, akibainisha kuwa kwa Wilaya hiyo kwa sasa vijiji 56 kati ya vijiji 59 vinapata huduma ya maji safi na ya uhakika, akibainisha kutambua changamoto ya maji kwenye vijiji vya Mpamantwa na Ibinwa.
Aidha akizungumzia tija ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa mkoani Dodoma, Dkt. Samia amesema kujengwa kwa reli na kituo cha SGR Wilayani Bahi pamoja na ujenzi wa bandari kavu kutaibadilisha Bahi kwa kiasi kikubwa na hivyo kuvutia uwekezaji pamoja na biashara, suala ambalo litakuza fursa za ajira kwa vijana wa Bahi na mkoa wa Dodoma kwa ujumla.
