Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa moja ya malengo makuu ya uongozi wake ni kuhakikisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitaacha deni la mkopo atakapomaliza muda wake wa uongozi.
Akizungumza Ikulu mjini Unguja na jopo la wahariri pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania Bara na Zanzibar, Dkt. Mwinyi alifafanua kuwa tayari Serikali imeweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa ulipaji wa madeni ili kuhakikisha deni la Serikali halibaki kuwa mzigo kwa vizazi vijavyo.
Dkt. Mwinyi alieleza kuwa Serikali imeanzisha akaunti maalum kwa ajili ya kulipa madeni ya mikopo, ambapo kila mwezi huwekwa kiasi cha dola za Marekani milioni 15. Hii ni tofauti na awali ambapo Serikali ilikuwa ikiweka dola milioni 10 pekee kwa mwezi.
Rais Mwinyi alisema kuwa mafanikio haya yanatokana na usimamizi mzuri wa fedha za umma na ongezeko la mapato kupitia kodi na ushuru, hali iliyowezesha Serikali kuwa na uwezo wa kukopesheka. Aliongeza kuwa kwa sasa taasisi nyingi za kifedha zinajitokeza kuikopesha Zanzibar kutokana na uaminifu uliojengeka kuhusu urejeshaji wa mikopo.
Rais Mwinyi pia alisisitiza kuwa mikopo inayochukuliwa na Serikali inalenga tu miradi ya maendeleo yenye tija, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, huduma za afya, elimu na nishati, ambayo ina matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.
Amesema kwamba uwazi, nidhamu ya matumizi ya fedha, pamoja na mipango ya kimkakati ya ulipaji wa madeni, ndiyo sababu Zanzibar inaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo huku ikiepuka kulemea bajeti ya taifa kwa madeni yasiyolipika.
@dr.hmwinyi
