
Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki, amefariki dunia.
Uhuru Kenyata, Rais wa sasa wa nchi hiyo, ametangaza kifo hicho leo Aprili 22, 2022 kupitia runinga mbalimbali nchini humo.
Kenyatta amesema Kibaki amefariki dunia usiku wa siku ya Alhamisi huku akimwelezea kuwa ni kiongozi aliyeimarisha demokrasia na hali ya uchumi kwa Wakenya.
Kibaki aliyemefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90, alikuwa rais wa tatu wa Jamhuri ya Kenya kutoka mwaka 2002 hadi 2013.
Rais Kenyatta amesema kiongozi huyo wa zamani wa taifa, ataandaliwa mazishi ya kitaifa na kwamba atakumbukwa kwa kuwezesha kupatikana Katiba ya Kenya mwaka 2010.
Kutokana na kifo hicho, Rais Kenyatta amesema bendera zote katika majumba ya umma, wizara na balozi zote za Kenya duniani zitapepea nusu mlingoti hadi atakapozikwa.
