
Rais wa Urusi Vladmir Putin amezihimiza nchi za Magharibi kuchukua hatua ya haraka ya kukidhi matakwa ya Urusi ya kuhakikishwa usalama na kuzuia utanuzi wa Jumuia ya Kujihami (NATO) kuelekea Ukraine na kupelekwa silaha za muungano huo wa kijeshi nchini humo.
Akizungumza katika kikao chake cha kila mwaka cha waandishi wa habari, kiongozi huyo wa Urusi ameyakaribisha mazungumzo na Marekani yanayotarajiwa kuanza Geneva mwezi ujao, lakini akaonya vikali kuwa Moscow inataraji mazungumzo hayo yatoe matokeo ya haraka.
Wiki iliyopita Urusi iliwasilisha rasimu za nyaraka zinazoitaka NATO kuinyima Ukraine uanachama pamoja na nchi nyingine za uliokuwa muungano wa Usovieti, na kupunguza idadi ya wanajeshi wanaopelekwa Ulaya ya Kati na Mashariki.
