Msimamizi wa Polisi Jamii kata ya Buyuni, manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, Elizaberth Mmbugu, amesema mauaji ya vijana waendesha pikipiki ni moja ya changamoto kubwa katika kata hiyo.
Amesema kutokana na matukio ya mauaji baadhi ya watu wanaogopa kununua pikipiki mpya huku madereva nao wakizikataa kuhofia usalama wa uhai wao.
Elizabert ameyasema hayo leo Agosti 9, 2022, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na MANDAI TV ONLINE ambapo anaomba jamii kufichua mtandao wa wanaonunua pikipiki hizo ili kukomesha vitendo hivyo vya kikatili na vinavyorudisha nyuma maendeleo.
“Kati ya mwezi Januari hadi sasa vijana wanne wameuawa katika matukio ya wizi wa pikipiki, wawili waliuawa Zavara, wengine Taliani na Buyuni,” amesema Elizaberth.
Hata hivyo, amesema katika kufuatilia matukio hayo wamebaini kuwa ili pikipiki iibiwe kuna makundi matatu ya watu wanaosababisha, ambayo ni watoa taarifa za pikipiki husika, wezi na wanaozinunua.
Aidha, amesema wakati wizi huo ukiendelea kubaki kitendawili, Polisi Jamii kata hiyo imesaidia kukomesha matukio ya wizi wa watoto, ukabaji na wizi wa majumbani uliokuwa umeshamili katika baadhi ya maeneo licha ya chamoto kubwa wanayokutana nayo ya kutolipwa posho zao kwa wakati kutokana na kazi hiyo.
