Paroko Joseph Musyoki wa parokia mpya ya Mtakatifu Yokimu na Ana, Zingiziwa, jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amefichukua kuwa hatua ya mwaamini kulitegemeza kanisa anajiwekea hazina duniani na mbinguni.
Baba Musyoki amesema hayo mwishoni mwa wiki iliopita katika kikao chake cha kwanza na Baraza la Walei la Barokia hiyo, linaoongozwa na mwenyekiti Mama Christa Mgembe.
Paroko Musyoki amesema mtu huyo atastawi kimaisha duniani na hazina nyingine ataikuta mbinguni baada ya kutwaliwa.
“Mtu anayelitegemeza kanisa anajiwekea hazina tangu duniani hadi mbinguni, Parokia kubwa mnazoziona leo zilianzia chini, hivyo tunapaswa kulitegemeza kanisa letu,” amesema.
Katika kikao hicho Paroko Musyoki na msaidizi wake Padri Lorand Kyomya wote wa kutoka shirika la Waparotini , walikutana na Baraza hilo pamoja na kufahamiana lakini pia kupanga mikakati ya kuiboresha parokia hiyo mpya iliyotangazwa na Baba Askofu mkuu,Juda Thadeus Ruwaich Julai 7, mwaka huu.
Miongoni mwa mikakati ambayo kikao hicho kiliazimia ni pamoja na kupanua jengo la kanisa lililopo sasa, kumalizia ujenzi wa vyoo, ujenzi wa sakristia, kumalizia nyumba ya mapadri na kujenga kikanisa chao eneo la nyumba hiyo pamoja ofisi ya muda.
Paroko Musyoki pia aliafikiana na Baraza hilo nia yake ya kutembelea Jumuia zote 20 za Parokia hiyo katika muda mfupi na kubariki nyumba za waamini wote wa kanisa hilo, na kwamba hilo amelianza rasmi Jumanne Agosti 9, 2022.
Pia kila Jumanne na Ijumaa kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 7:00 mchana atakuwa akisikiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa waamini wake kanisa hapo.
Aidha, ameonesha nia yake ya kuiendelea parokia hiyo kwa kusaidiana na Baraza hilo la Walei ambalo alilielezea kuwa linajitahidi kuwajibika kutekeleza majukumu yake ikiwamo ya ujenzi wa nyumba ya mapadri ambalo lilisimamia kabla.
