
Rais wa zamani wa Pakistan na mtawala wa kijeshi wa Nchi hiyo, Pervez Musharraf, jana aliswaliwa swala ya mwisho mjini Karachi.
Ibada hiyo ilifanyika katika uwanja wa kambi ya kijeshi saa chache baada ya mwili wake kusafirishwa kwa ndege maalum hadi mji wa bandari wa kusini kutoka Dubai, ambako yeye na familia yake walikaa miaka yake ya mwisho katika uhamisho wake.
Miongoni mwa waliohudhuria ni wakuu wa zamani wa kijeshi Qamar Javed Bajwa, Ashfaq Parvez Kayani na Aslam Beg.
Waziri Mkuu wa sasa Shehbaz Sharif hakuhudhuria, lakini alitoa ujumbe wa rambirambi kwenye Twitter akisema “natoa rambirambi zangu kwa familia ya Jenerali Pervez Musharraf. Roho ya marehemu ipumzike kwa amani!
Musharraf alizikwa katika makaburi ya kijeshi huko Karachi.
Musharraf alifariki dunia Jumapili huko Dubai akiwa na umri wa miaka 79 kutokana na amyloidosis, ugonjwa adimu ambapo protini isiyo ya kawaida hujilimbikiza kwenye viungo, na kusababisha kutofanya kazi vizuri.
Aliingia madarakani Oktoba 1999 baada ya kumpindua Waziri Mkuu aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia Nawaz Sharif, kaka wa waziri mkuu wa sasa, katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu.
