“Tunasikia Oktoba Tunatiki na No Reform, No Election niwaambie Sisi kama Jeshi la Polisi tunafanyia kazi kauli hizi, mfano Mtu akisema Hakuna mabadiliko hakuna Uchaguzi nitamuuliza kwa Sheria ama kanuni zipi? Unaposema No Reform, No Election kwa sheria ipi? Kushindwa kusema ni sheria ipi maana yake unanipa nafasi ya kukukataza ambalo ni jukumu langu, ila unaposikia Oktoba tunatiki kwa kigezo cha alama unafahamu ni haki ya Kikatiba, ipo kisheria” hayo ni maneno ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linafahamu umuhimu wa kuwepo mazingira ya amani, utulivu, haki, na kuheshimu misingi ya demokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Alikuwa akizungumza jana Agosti 20,2025, katika mdahalo uliohusu amani, haki, na demokrasia uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
“Serikali zinazoundwa lazima ziwe za watu na zitokane na matakwa ya kidemokrasia. Kila raia ana haki ya kushiriki katika shughuli za umma, kuteua na kuteuliwa. Uhuru wa mawazo na maoni ni haki ya kikatiba, hata wakati wa uchaguzi,” amesema Kamanda Muliro.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya usalama na litasimamia masuala ya haki, amani, na utulivu, huku likipambana na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kusababisha vurugu wakati wa uchaguzi.
Pia, Kamanda Muliro amewakumbusha wananchi kuhusu wajibu wao wa kutii sheria na kulinda amani ya Taifa.
“Suala la ulinzi wa Taifa ni jukumu la kikatiba. Jeshi la Polisi lipo kuhakikisha usalama wa watu na mali, lakini kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani ya nchi yake,” amesisitiza Kamanda Muliro.
