
Idadi ya watoto wadogo wanaokabiliwa na utapiamlo sugu nchini Somalia imeongezeka na kufikia zaidi ya nusu milioni mwaka huu.
Umoja wa Mataifa unasema hiyo ni kiwango cha juu zaidi kuliko ilivyokua wakati wa njaa mwaka 2011 ambapo maelfu ya watoto walifariki dunia.
James Elder, msemaji wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, anasema kuna watoto zaidi ya nusu milioni wanaokabiliwa na kifo kinachoweza kuzuilika kutokana na ukosefu wa chakula.
Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva jana Jumanne, Elder amesema kiwango hicho cha watoto kukabiliwa na utapiamlo hakijawahi kushuhudiwa katika karne hii wala katika nchi yoyote duniani.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba baadhi ya maeneo ya Somalia yatakumbwa na hali sugu ya njaa katika miezi ijayo wakati pembe ya Afrika ikishuhudia msimu wa tatu mfululizo bila ya kunyesha mvua.
Njaa iliyokumba Somalia 2011 ilizababisha zaidi ya vifo vya watu robo milioni, nusu wao wakiwa ni watoto.
Elder anasema kuna watoto laki 513000 chini ya miaka mitano wanaotazamiwa kukabiliwa na utapiamlo ikimanisha wanaweza kufariki kutokana na magonjwa kama vile surua, malaria na kipindupindu, magonjwa yanayosambaa nchini humo hivi sasa.
Shirika la Afya Duniani WHO, wiki iliyopita ilitangaza kwamba mamia ya watu huenda wamefariki kutokana na njaa, hali ambayo inatokea chini ya miaka 10 iliyopita.
Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alionya kwamba sehemu kubwa ya Somalia itatumbukia katika hali ya njaa ikiwa wafadhili hawatatoa msaada unaohitajika haraka iwezekanavyo.
