
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema maeneo ya Mapori Tengefu yatakayopandishwa hadhi kuwa Mapori ya Akiba ni yale yenye hadhi nzuri kwa ajili ya uhifadhi na yasiyo na vijiji vya wananchi.
Masanja ameyasema hayo jana Juni 20, 2022, Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka iwapo Serikali itayapandisha hadhi maeneo ya wananchi.
“Hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii iligusia upandishwaji hadhi maeneo ambayo hayatahusisha vijiji vya wananchi, hivyo maeneo yanayokwenda kupandishwa hadhi kutoka mapori tengefu kuwa mapori ya akiba ni muhimu tu kwa ajili ya uhifadhi na hayana wananchi ndani yake,” amesisitiza Masanja.
Amesema maeneo hayo ya mapori tengefu kutokana na umuhimu wake, kwa asilimia kubwa yanatumika kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na utalii.
Amebainisha kuwa Serikali inapoona pori tengefu lina hadhi nzuri na sifa ya kuhifadhiwa zaidi kwa maslahi ya taifa hulipandisha hadhi kutoka pori tengefu kuwa pori la akiba vivyo hivyo pori la akiba linapoongezeka sifa linapanda kuwa hifadhi ya Taifa.
Aidha, Naibu Waziri huyo amewaomba wabunge ambao maeneo yao wanaopakana maeneo hayo wawe na uelewa wa pamoja huku akisisitiza kuwa ardhi ni mali ya umma na si ya mtu mmoja akiwaomba waache kutumia kauli zinazoweza kuwagawa wananchi.
