Shirika la Afya Duniani (WHO), limeonya kuhusu mahitaji makubwa ya huduma za afya katika maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina baada ya mzozo wa mwezi uliopita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.
Ofisi ya shirika hilo kanda ya Mediterania Mashariki, katika taarifa yake hapo jana imesema WHO inaimarisha juhudi zake za kutoa msaada wa afya kwa watu takriban 200,000 wenye mahitaji katika maeneo yote ya Wapalestina, ukiwemo Ukingo wa Magharibi.
Rik Peeperkorn wa WHO amesema hali ni tete na shirika hilo lina wasiwasi mkubwa na linataka liruhusiwe bila vizuizi kupeleka misaada ya kibinadamu na maendeleo na wafanyakazi wake katika Ukanda wa Gaza na liweze kuwasafirisha wagonjwa katika hospitali nyingine nje ya Gaza kwa matibabu zaidi itakapohitajika.
Taarifa ya WHO imesema watu zaidi ya 77,000 walilazimika kuyakimbia makazi yao na vituo takriban 30 vya afya viliharibiwa wakati wa vita vya siku 11, ambapo Wapalestina 254 wakiwemo watoto 66 waliuliwa.
Peeperkorn amesema maisha ya Wapalestina yanaendelea kuzorota huku wengi walioathiriwa na mzozo huo wakihitaji msaada na wakikabiliwa na vitisho vingine vya afya kama ugonjwa wa COVID-19.
