
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Pugu Bombani, manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, Amanzi Bungala, amesema anatembea kifua mbele baada ya kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mtaa wake.
Akizungumza na Mandai TV Online jana Bungalaametaja miradi iliyotekelezwa kwa usimamizi wake kuwa ni pamoja na maji, umeme, usafi wa mazingira, urasimishaji, michezo na burudani.
“Changamoto ya maji katika mtaa huu ilikuwa ni kubwa wakati naingia madarakani, nimesimamia kuhakikisha maji yanapatikana sasa asilimia 99 wananchi wangu wanapata maji safi na salama,” amesema.
Hata hivyo, amebainisha kuwa maeneo ya Kwa mjumbe Nyasulu na Tegemea hadi mwishoni mwa Agosti nao watakuwa wamepata maji safi na salama ya Dawasa.
Kuhusu ulinzi na usalama, Mwenyekiti Bungala amesema mtaa huo uliathiriwa na panyaroad, hivyo kwa kushirikiana na polisi wamedhibitiwa na sasa hali ni shwari.
“Tumeungana na RC wetu wa Dar es Salaam kuwa panya road aliyeko shimoni abaki huko huko, nasi tunaendelea kulinda mtaa wetu ili uendelee kubaki salama,” amesema.
Bungala amesema awali madereva bodaboda nao walikuwa tishio kwa usalama ambapo walikuwa wakihusika na vitendo vya uhalifu lakini sasa hali ni shwari.
Kuhusu usafi wa mazingira, amesema amewahamasisha wananchi wake kwa kushirikiana na ofisa mtendaji na wajumbe kufanya usafi wa mazingira kwenye kila kona ya mtaa huo wamefanikiwa.
“Tuna kampuni ya uzoaji taka ya Zunzu investment inayojishughulisha na uzoaji taka, hadi mwezi Septemba tunataka Pugu Bombani ing’are,” amesema.
Kuhusu umeme amesema umeme wa Rea umesambazwa katika maeneo mengi ya mtaa huo.
Katika sekta ya michezo na burudani Bungala amesema ameanzisha matamasha ya vijana ambayo yanatoa burudani kwa wananchi wake mara nyingi.
“Nilianzisha kombe la jezi mshindi alipatikana, nikaanzisha kombe la mbuzi nalo liliisha vizuri, lengo la kuanzisha makombe haya nataka baada ya kazi, jioni wananchi wangu waburudike.
“Pia tunatafuta vipaji, tumepata vijana 18, wameunda timu yao, kabla nilikusanya vikundi vya wazee ili wacheze ngoma zao za makabila lakini wengi wao walishindwa kuendeleza ngoma hizo.
Bungala amesema katika suala la urasimishaji linaendelea vizuri miongoni mwa waliopimiwa wamepata hati zao.
Kuhusu mchakato wa Sensa na Watu na Makazi, Bungala amesema mtaa huo unasubiri siku ya kuhesabiwa uhesabiwe.
Tumehamasisha wakazi wetu wote kuhesabiwa, tunasubiri Agosti 23, ije tuhesababiwe. Nina uhakika wana-Bombani wote tutahesabiwa na idadi yetu itajumuishwa miongoni mwa Watanzania wote.
