MWANZA
Mwanamke mmoja aliye fahamika kwa jina la Warioba Lucas, maarufu ‘Wevi’ (41) Mkazi wa kitongoji Cha Nyakasege wilayani Magu Mkoa wa Mwanza amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani humo akiuguza majeraha ya moto aliyoyapata baada ya kujimwagia mafuta ya Petroli kisha kujichoma moto.
Warioba anadaiwa kujitendea unyama huo Jumatatu Agosti 26, 2024, saa 5 asubuhi, siku moja baada ya mume wake kudaiwa kuchukua Sh40,000 aliyoitumia kunywa pombe, jambo lililomkera.
Akitoa taarifa hiyo Jumanne Agosti 27, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mwanamke huyo alifikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na tabia za mume wake, Jumanne Ngika (45) kuchukua fedha za familia kwenda kuzitumia kwa ulevi na starehe nyingine.
Kamanda Mutafungwa amesema baada ya Warioba kujichoma moto, wananchi walibaini tukio hilo na kuvunja mlango wa chumba alimokuwemo kisha kuanza kuuzima moto uliokuwa umeshasambaa kwenye mavazi yake kwa kutumia maji na mchanga na kufanikiwa kuuzima. Hata hivyo, alikuwa ameshaungua sehemu mbalimbali za mwili.
