Bilionea na mwanzilishi wa kampuni ya SpaceX, Elon Musk, ametangaza mpango wa kutoa hisa moja ya kampuni hiyo kwa kila mtoto nchini Marekani kuanzia mwaka 2027. Musk ametoa ahadi hiyo kupitia mtandao wa kijamii wa X, ingawa hajaeleza kwa kina namna hisa hizo zitakavyogawiwa au utaratibu utakaotumika kutekeleza mpango huo.
Musk hakufafanua iwapo kila mtoto atapokea hisa moja moja moja kwa moja, wala kama kutakuwa na masharti ya umri, uraia au usimamizi wa hisa hizo. Pia, hakutoa maelezo kuhusu thamani ya hisa moja au gharama ya jumla ya kutekeleza ahadi hiyo kwa mamilioni ya watoto wanaoishi nchini Marekani.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amepongeza tangazo hilo akieleza kufurahishwa na kile alichokiita ukarimu wa Musk. Trump amesema mchango huo utatolewa kupitia mpango wa TRUMP ACCOUNTS, ingawa maelezo zaidi kuhusu namna akaunti hizo zitakavyohusiana na hisa za SpaceX hayajawekwa wazi.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Sensa ya Marekani, nchini humo kuna takribani watoto na vijana milioni 73 walio chini ya umri wa miaka 18. Ikiwa ahadi hiyo itatekelezwa kwa watoto wote wanaolengwa, itahusisha idadi kubwa ya wanufaika na kuhitaji utaratibu maalumu wa usajili, ugawaji na usimamizi wa hisa hizo.
SpaceX ni kampuni ya teknolojia ya anga inayomilikiwa na Musk, inayojihusisha na kurusha roketi, kusafirisha vifaa na wanaanga angani pamoja na huduma za intaneti kupitia mtandao wa Starlink. Kampuni hiyo pia imekuwa ikitajwa katika mipango ya uwezekano wa kuuza hisa kwa umma, jambo linaloweza kuathiri namna thamani ya umiliki wake inavyopimwa.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna maelezo ya kutosha yaliyotolewa kuhusu masharti ya mpango huo, namna hisa zitakavyohamishwa au kama ahadi hiyo imewekewa utaratibu rasmi wa kisheria. Utekelezaji wake utategemea maelezo zaidi kutoka kwa Musk na wahusika wa mpango wa TRUMP ACCOUNTS.
