
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango anashiriki mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 unafikia tamati leo nchini Sweden.
Katika mkutano huo, viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa wametoa ahadi pamoja na mapendekezo mbalimbali ya namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira duniani.
Akizungumza katika mkutano huo jana Juni Pili, 2022, Dk. Mpango amesema ili kuhakikisha dunia inakuwa salama kwa viumbe wote wanaoishi, hakuna budi kutekeleza kikamilifu makubaliano mbalimbali ya kimataifa ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.
Amesema makubaliano hayo ni pamoja na yaliofanyika Rio de Jeneiro, Paris, Kyoto pamoja na Glasgow.
Dk Mpango ameongeza kuwa kinachohitajika ni utayari wa kisiasa pamoja na jitihada za pamoja katika kukabiliana na changamoto hizo ambazo zinasababishwa na shughuli za binadamu.
Aidha, Makamu wa Rais amesema Tanzania imefanya jitihada mbalimbali katika kupambana na uharibifu wa mazingira ikiwamo kulinda misitu ya asili pamoja na juhudi za kitaifa za upandaji miti huku ikienda sanjari na kuhifadhi kilometa za mraba 307,800 ambazo ni sawa na asilimia 32.5 ya eneo lote la nchi kwa ajili ya Hifadhi za Taifa pamoja na misitu.
Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania katika teknolojia rafiki kwa mazingira ikiwamo teknolojia zinazoweza kubadili taka kuwa nishati ya gesi na mbolea.
Pia amewaalika watafiti kutoka mataifa yalioendelea kushirikiana na kampuni pamoja na watafiti wa ndani nchini Tanzania kwa kuendeleza teknolojia rahisi na rafiki kwa mazingira katika kutumia nishati ya jua na upepo iliopo nchini.
Halikadhalika amesema pamoja na Tanzania kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira bado suala hilo lipaswa kupewa kipaumbele na mataifa yote kwani juhudi za Tanzania pekee hazitoweza kukabiliana na changamoto hiyo duniani.


