
Meya wa manispaa ya Shinyanga, David Nkulila, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Jumatatu Agosti 23,2021 wakati akipatiwa matibabu, katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Nkulila ambaye ni Diwani wa kata ya Ndembezi (CCM), tangu mwaka 2010, na Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mwaka 2010-2015, alichaguliwa kuwa meya wa manispaa hiyo, Novemba 24, mwaka jana 2020, baada ya kupata ushindi kwa mara ya tatu na ametumikia nafasi hiyo katika kipindi cha miezi 10 hadi umauti ulipomkuta.
Msemaji wa familia ya marehemu Nkulila, Mary Joseph, akizungumza na wanahabari leo asubuhi, amesema mjomba wake amefariki dunia saa 11 alfajiri kutokana na maradhi ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Amesema msiba upo nyumbani kwa marehemu eneo la Mabambasi, kata ya Ndembezi jirani na Kanisa la Moravian na kwamba mazishi yake yatafanyika Jumatatno Agosti 25, mwaka huu.
