
Mkuu wa Makanisa ya Power of God Tanzania, Askofu Dankton Rweikila, amesema changamoto ya kukosa kazi, watoto, ndoa, biashara kuyumba na umaskini zinasababishwa na kufungwa vitovu.
Baba askofu Rweikila ametoa kauli hiyo jana Agosti 22, 2021, Dar es Salaam, wakati wa mahubiri yake na amewataka wanaokabiliwa na changamoto hizo na nyingine wafike katika madhabahu ya kanisa hilo, lililoko Chanika eneo la Sheraton, ambapo kwa jina la Yesu, waliofungwa na vifungo mbalimbali wanafunguliwa.
Amefafanua kuwa watu waliofungwa vitovu vyao wanapofanya biashara hawapati faida, wanaofanya mazuri jamii hawayaoni, wamesoma lakini wanahangaika kutafuta kazi, ni warembo lakini hawapati ndoa na pia wanahangaika kutafuta watoto.
Aidha, amefafanua kuwa watu wamekuwa wakifungwa vitovu vyao wakati wa kuzaliwa, wa ndoa au matukio mbalimbali ambapo babu, bibi au jamaa yeyote anaweza kutumia fursa hiyo kufunga vitovu wengine na hivyo kuwafanya washindwe kufanikiwa katika kila jambo wanalofanya.
Sanjari na mahubiri hayo ameliombea kusanyiko kubwa lililohudhuria kanisani hapo, ambapo 21 miongoni mwao waliofungwa vitovu vyao walifunguliwa kwa jina la Yesu kupitia maombi hayo.
Baba Askofu Rweikila amesema kwa Mungu kila kitu kinawezekana kwa imani, hivyo madhabahu ya kanisa hilo imekuwa ikiamini hilo na imekuwa ikiliitia jina la Yesu na matatizo mengi yanayowakabili wanajamii kufunguliwa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Makanisa ya Power of God ameweka wakfu na kuzindua vitabu viwili NJIA ZA UZIMA ANAZO BWANA na MAOMBI YENYE NGUVU YA KUTEKA BARAKA, alivyotunga.
Katika kitabu NJIA ZA UZIMA ANAZO BWANA kinachouzwa kwa shilingi 3000, amesema roho za huzuni na upweke zinazowatesa baadhi ya watu, zitatoweka kwa kukisoma.
Katika KITABU MAOMBI YENYE NGUVU YA KUTEKA BARAKA ambacho kinauzwa kwa shilingi 2000, kila atakayesoma na kukinenea akitakacho kitatokea.
