
Miili saba zaidi imetolewa kutoka mto Yala Magharibi mwa Kenya karibu na mahali ambapo makumi ya wengine zaidi wamegunduliwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Ripoti ya polisi iliyoonekana na maofisa katika hifadhi ya maiti ya kaunti ndogo ya Yala, miili ambayo haikudaiwa na yeyote ilitolewa mtoni katika muda wa miezi miwili iliyopita.
Miili hiyo haijatambuliwa huku ikisubiri kufanyiwa uchunguzi.
Maofisa wa chumba cha kuhifadhi maiti wanasema miili mitatu ilitolewa na wapiga mbizi mwezi Septemba na mingine minne iligunduliwa na wakazi kando ya mto huo.
Ugunduzi wa hivi punde unaongeza idadi ya miili iliyochukuliwa kutoka mtoni hadi zaidi ya 30 tangu Januari mwaka huu.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema wakazi katika eneo hilo wanaishi kwa hofu kutokana na kupatikana kwa miili isiyojulikana kutoka kwenye mto huo.
Polisi bado hawajatoa maoni yao kuhusu suala hilo.
Maelezo ya uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa mapema mwaka huu kutaka kubaini ni nani alihusika na sababu za mauaji hayo bado hazijawekwa wazi.
Kumekuwa na wasi wasi kuhusu visa vya utupaji miili katika mito ya Kenya siku za hivi karibuni.
Septemba iliyopita, miili 11 iligunduliwa katika Mto Tana katika Kaunti ya Garissa Kaskazini-mashariki mwa Kenya.
